Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Bi. Dkt. Fatemeh Bostan, mjumbe mwanzilishi wa Chama cha Haki cha Uturuki, katika warsha-pepe ya tano ya kimataifa isemayo: "Iran; Jukwaa la Heshima ya Kiislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni," iliyoandaliwa kwa juhudi za Majma‘u-l-‘Ālamī Qādimūn, alisisitiza umuhimu wa nafasi ya Iran katika mizani ya nguvu za kikanda na msaada endelevu kwa mapambano ya Palestina.
Bi. Dkt. Fatemeh Bostan, akirejelea uendelevu wa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuilinda Palestina, alisema: Iran tangu mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi hadi leo, imekuwa na msimamo thabiti, wa kimsingi na unaotegemea mafundisho ya kidini dhidi ya uvamizi wa Kizayuni.
Akiikosoa mienendo ya taasisi za kimataifa, aliongeza: Tangu kuanzishwa kwa utawala wa Kizayuni, utawala huu kwa kupuuza sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, umesababisha migogoro mingi katika eneo. Umoja wa Mataifa, ambao ulipaswa kuwa mdhamini wa amani duniani, haujaweza kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya Israel, na maamuzi mengi ya kisheria na ya kimahakama kwa vitendo yamepuuzwa.
Mjumbe mwanzilishi wa Chama cha Haki cha Uturuki, huku akigusia vikwazo na mashinikizo ya kijeshi dhidi ya Iran, alisisitiza: Uzoefu wa miaka ya hivi karibuni umeonesha kuwa Iran, licha ya vikwazo vya kiuchumi na vitisho vya nje, ina mshikamano wa ndani na uwezo mkubwa wa kujilinda. Aina yoyote ya shinikizo au hatua ya kijeshi, sio tu kwamba haitasababisha kubadilika kwa mfumo au kusimamishwa kwa mipango halali ya Iran, bali pia itabadilisha mizani ya nguvu za kikanda kwa manufaa ya mhimili wa muqawama.
Aliiona nafasi ya Iran katika msaada wa kivitendo kwa muqawama wa Palestina kuwa ya umuhimu mkubwa, na akasema: Misaada hii inapaswa kuwa chachu ya umoja wa Umma wa Kiislamu na kuzuia kuibuka kwa migawanyiko ya kimadhehebu na kisiasa kati ya nchi za Kiislamu. Kutetea haki za watu wa Palestina ni suala la msingi na lisiloweza kujadiliwa, na linapaswa kupewa kipaumbele kama ajenda ya kimataifa.
Dkt. Bostan katika kuendelea, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya kikanda na akasema: Uzoefu wa kihistoria unaonesha kuwa ni kupitia njia ya mazungumzo, mshikamano na ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu pekee ndipo uthabiti na usalama wa kudumu wa eneo vinaweza kuhakikishwa. Iran, kwa misimamo yake ya kimsingi, imewasilisha mfano wa vitendo kwa nchi nyingine za Kiislamu.
Warsha-pepe hii ilifanyika kwa ushiriki wa wanafikra, wahadhiri wa vyuo vikuu na wawakilishi wa kisiasa kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu, na mada kuu zilikuwa ni kuchunguza nafasi ya Iran katika kukabiliana na uvamizi wa Kizayuni, kuunga mkono muqawama wa Palestina, kulinda uthabiti wa eneo na kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu.
Maoni yako